Saturday, 21 September 2013

WATU 39 WAMEFARIKI NA WENGINE TAKRIBAN 150 WAMEJERUHIWA NAIROBI KATIKA DUKA LA WESTGATE



Duka la kifahari lililoshambuliwa la Westgate katika mtaa wa Westlands Nairobi.

Al shabaab: ''Kenya ilipuuza onyo letu''
Afisaa mmoja mkuu wa kundi la kigaidi la Alshabaab, amesema kuwa kundi hilo ndilo limehusika na shambulizi dhidi ya duka la kifahari la Westgate mjini Nairobi Kenya.

Kwa mujibu wa Afisaa huyo mashambulizi hayo yalikuwa ya kulipiza kisasi kwa Kenya kwa kujihusisha na vita vya Somalia ambako wanajeshi wake wanakabiliana na kundi hilo.



Wanajeshi wa Kenya wamekuwa nchini humo tangu mwaka 2011 kama sehemu ya juhudi za muungano wa Afrika kutaka kurejesha uthabiti nchini Somalia.

Taarifa kutoka Ikulu ya Rais Kenya zinasema kuwa mshukiwa mmoja aliyekamatwa alifariki kutokana na majeraha yake.
 

Baadhi ya watu waliofanikiwa kukimbilia usalama wao

Wanamgambo wa Al Shabaab kupitia kwa mtandao wao wa Twitter , wanasema kuwa Kenya haikuchukulia kwa uzito onyo walilotoa kwa taifa hilo kwa hatua ya kuwapeleka wanajeshi wake nchini humo kupambana dhidi yao.

Kundi hilo limesema limekuwa likitoa onyo mara kwa mara kwa Kenya kuwa ikiwa haitaondoa vikosi vyake nchini Somalia, athari zitakuwa mbaya mno.

Kupitia mtandao wao wa Twitter, Al Shabaab limesema kuwa Kenya ilijidai kutosikia onyo hizo, na kuendelea kuwaua waisilamu wasio na hatia nchini Somalia.
Taarifa hiyo ya Twitter ilisema kuwa Shambulio la Westgate ni tone tu katika bahari ya mfano wa yanayowakumba wasomali nchini Somalia.

Taharuki ilianza hii jana saa saba mchana wakati watu wanaokisiwa kuwa kumi walipovamia jengo la kifahari la Westgate na kuwapiga risasi kiholela wakenya waliokuwa wanaendelea na shughuli zao za kawaida.